http://tropicalpoultryfarming.blogspot.com/

Azam fc yang'ara ligi ya mabingwa afrika yaitandika Al Merreikh

Akitokea benchi, John Bocco alifunga bao la pili katika dakika ya 78 akiunganisha kwa kichwa kona ya nahodha Salum Abubakar

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Azam FC jana wameanza vyema kampeni ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufunga Al Merreikh ya Sudan kwa mabao 2-0.
Mbele ya maelfu ya mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Azam FC iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya tisa likifungwa na Didier Kavumbagu.

Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Burundi alifunga bao la kwanza baada ya kutumia makosa ya mabeki wa klabu hiyo ya Khartoum na kipa wao, Magoola Salum, raia wa Uganda, ambaye mpira uliogonga miguu na kisha ukarudi tena kumgonga beki wake mmoja kabla ya Kavumbagu kuujaza wavuni.

Akitokea benchi, John Bocco alifunga bao la pili katika dakika ya 78 akiunganisha kwa kichwa kona ya nahodha Salum Abubakar. Huo ulikuwa mpira wa kwanza kuugusa Bocco uwanjani tangu aingie kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwingine, Kipre Tchetche wa Ivory Coast.

Kwa matokeo hayo dhidi ya moja ya timu mahiri Afrika, Azam FC inahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga mbele katika michuano hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza baada ya kuwa bingwa wa Bara msimu wa 2013/2014.

Wageni walianza pambano la leo kwa kasi na walipoteza nafasi nzuri katika dakika ya pili iliyopotezwa na mchezaji wake, Babeker Bakri, kabla ya Azam FC kuzinduka katika dakika za nne na saba wakati Tchetche alipopoteza nafasi nzuri kwa mashuti yake kudakwa na kipa Salim wa El Merreikh.

Baada ya bao la Kavumbagu, El Merreikh walikosa bao katika dakika ya 21, baada ya Mkenya Allan Wanga kupiga shuti kali baada ya kupokea pasi ya Abdallah Ragei. Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu.

Dakika ya 35, Tchetche alishindwa kumtengenezea nafasi nzuri Kavumbagu afunge bao la pili baada ya kipa wa El Merreikh kutoa pasi ya nyuma huku Mrundi huyo akiwa mbele. Dakika mbili baadaye, Tchetche alipiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari ambalo lilitoka nje ya goli.

Azam FC ilikwenda mapumziko ikiwa mbele, na kipindi cha pili kilianza kwa El Merreikh kufanya mabadiliko kwa kumtoa Kamal Amir na kuingia Mogame Traore.

Dakika nne baada ya kuanza kipindi hicho, Wanga alioneshwa kadi ya njano na mwamuzi Hassan Mohammed wa Somalia kwa kushika mpira kwa makusudi, huku Aggrey Morris naye akioneshwa kadi hiyo kwa kucheza rafu.

El Merreikh walikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupoteza nafasi mbili nzuri za mabao, lakini Azam nao wakipoteza nafasi nzuri kupitia kwa nahodha Abubakar, kabla ya kumtoa Frank Domayo na kuingia Himid Mao.

Dakika ya 62, kipa wa Azam FC, Aishi Manula aliokoa mpira wa tik-tak wa Traore, kabla ya beki Erasto Nyoni kukaribia kuifungia timu ya Chamazi baada ya shuti lake kugonga mlingoti wa juu wa lango na kutoka nje. Dakika mbili baadaye, Kavumbagu alikosa bao akiwa amebaki na kipa wa El Merreikh.

Baada ya hapo, na hasa baada ya kuingia Bocco, Azam FC inayofundishwa na Joseph Omog wa Cameroon ilizidi kutakata kwa kulishambulia kwa nguvu lango la El Merreikh kabla ya kumuingiza Amri Kiemba katika dakika ya 86 akichukua nafasi ya Kavumbagu.

Labels:

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

CHARLES CHAMI. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget