KLABU ya Simba imesema kuwa imewabaini wachezaji wake waliocheza chini ya kiwango hadi timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba ambayo tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti ilikuwa haijafungwa hadi wiki moja iliyopita ilipopata vipigo mfululizo, imesema itawachukulia hatua wachezaji hao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema timu yao ilipoteza mechi hizo mbili baada ya baadhi ya wachezaji kucheza chini ya kiwango.
Amesema timu yao itawachukulia hatua za kinidhamu wachezaji hao waliocheza chini ya kiwango.
Awali, timu hiyo ilipokea kichapo cha kushtua cha bao 1-0 kutoka kwa timu iliyopanda daraja ya African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru kabla ya kulambwa 2-1 na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.
Hatahivyo, Hans Poppe hakuwataja wachezaji hao wanaodaiwa kucheza chini ya kiwango na kusababisha timu hiyo inayoongoza ligi kupunguza pointi hadi kubaki mbili dhidi ya watani wao Yanga.
Kimsimamo, Simba wana pointi 35 wakati Yanga sasa wamefikisha pointi 33 na kubakisha pointi mbili tu kabla ya kuikuta Simba.
Aidha, Simba pia imedai kuwa timu yao imekuwa ikifungwa kutokana na mbinu chafu za nje ya uwanja.
Akinukuliwa katika mtandao mmoja, Hans Poppe alisema baada ya mwanzo mzuri katika Ligi Kuu, ikiwemo kuwazuia mabingwa watetezi, Yanga kwa sare ya 1-1 wapinzani wao wakaanza mchezo mchafu.
“Hebu jiulizeni, Simba ni timu nzuri tangu mwanzo inacheza vizuri na kushinda, Tumecheza mechi na hao mabingwa, tukiwa pungufu baada ya Mkude (Jonas) kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini tukasawazisha bao na refa akakataa bao letu lingine. Iweje ghafla tufungwe mechi mbili mfululizo?” alihoji.
Alisema kuna mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani wao na hayo yamekuwa yakijirudia kwa miaka mitano sasa, jambo ambalo ni hatari kwa soka la Tanzania.
Simba SC ilianza vyema Ligi Kuu na kuongoza kwa muda mrefu ikicheza mechi 13 bila kupoteza, ikishinda 11 na sare mbili. Lakini ghafla kibao kikageuka kwenye raundi mbili za mwisho na timu hiyo ikapoteza mechi mbili mfululizo.
Hatahivyo, pamoja na kufungwa mechi mbili mfululizo Simba bado imemaliza duru la kwanza ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.
Post a Comment