Katika mchezo wa
kwanza uliofanyika kwenye uwanja huohuo wa Azam Complex Azam walilala kwa bao
1-0 mbele ya vijana wa kocha Fredy Minziro kitu ambacho kinaashiria ugumu wa
mchezo
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania
bara, Azam FC, leo Jumamosi, wanatarajia kushuka kwenye dimba lao la Azam
Complex kuwakabili Maafande wa JKT Ruvu, kutoka mkoani Pwani.
Azam ambao Jumamosi iliyopita waliondoshwa
kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na El Merreikh, bila shaka itaingia
katika mchzo huo ikiwa na hasira za kutaka kupoza machungu yake na kupunguza
idadi ya pointi kati yao na vinara wa ligi hiyo Yanga.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye
uwanja huohuo wa Azam Complex Azam walilala kwa bao 1-0 mbele ya vijana wa
kocha Fredy Minziro kitu ambacho kinaashiria ugumu wa mchezo huo wa kesho.
Kabla ya kutolewa na El Merreikh kwenye
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Azam ilicheza mechi mbili za ligi dhidi ya
Ruvu Shooting na Tanzania Prisons na zote ilipata sare ya bila kufungana huku
JKT Ruvu nayo ikienda sre ya 1-1 na Tanzania Prisons Jumamosi iliyopita kwenye
uwanja huo wa Azam Complex.
Kocha wa muda George Nsimbe ‘Besti’ huo
utakuwa mtihani wake wa kwanza kukiongoza kikosi cha Azam akiwa mkuu wa benchi
la ufundi baada ya kukabidhiwa mikoba hiyo Jumatatu ya wiki hii kufuatia
kutimuliwa kwa kocha mkuu Joseph Omog.
Nsimbe atahakikisha anatumia silaha zote
muhimu kwa ajili ya kupata ushindi katika mchezo huo ili kurudisha matumaini ya
timu hiyo kutetea ubingwa wao wa ligi ya Vodacom ili kupata nafasi ya kushiriki
michuano ya kimataifa mwakani.
Kwaupande wao JKT Ruvu waliopo kwenye nafasi
ya 10, watahakikisha wanapambana na kupata ushindi ili kujinasua na janga la
kushuka daraja msimu huu.
Washambuliaji Idd Mbaga Reliants Lusajo na
Amosi Mgisa watakuwa na kazi moja tu ya kulitia msukosuko lango la Azam ambalo
asilimia kubwa ya wachezaji wake wanaonekana kutokuwa sawa baada ya ndoto zao
kupotea katika michuano ya ligi ya Mabingwa Afrika.
Bilashaka kocha Nsimbe atataka kumpumzisha
kipa wake chipukizi Aishi Manula kwenye mchezo huo na kumtumia mkongwe, Mwadin
Ali huku akiendelea kuwatumia washambuliaji wake Didier Kavumbagu, Kipre
Tchetche ambao wameonyesha uelewano mkubwa msimu huu sambamba na wingi Brian
Majwega.
Pamoja na kuhakikishiwa kibarua chake na
uongozi wa timu ya Azam lakini faraja pekee kwa kocha George Nsimbe ni kupata
pointi tatu ambazo zitairudisha timu hiyo katika mbio za kutetea ubingwa na
kuitia wasiwasi Yanga inayoongoza ligi hiyo kwa sasa.
Post a Comment