Kocha Mserbia Goran Kopunovic bado haja kiongoza kikosi cha Simba dhidi ya Yanga na leo itakuwa mara yake ya kwanza kuonja presha ya pambano la watani hao wa jadi
SIMBA na Yanga zinakutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mechi ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa pande zote mbili kutokana na upinzani wa klabu hizo na historia zao kwenye soka la Tanzania.
Yanga haijapoteza mchezo wa ligi mbele ya watani wa Simba huu ukiwa ni msimu wa tatu mfululizo na mchezo ujao wa ‘Dar es Salaam Derby’ utakuwa ni mchezo wa sita kuzikutanisha timu hizo kwenye ligi kwa misimu mitatu ya hivi karibuni.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga kwenye mechi za ligi kuu ilikua Mei 7 2012 ambapo Simba ilichomoza na ushindi mkubwa zaidi baada ya kuisukuma Yanga kwa goli 5-0 na kutwaa ubingwa wao wa mwisho kwenye ligi kuu Tanzania bara.
Yanga wao wamefanikiwa kuifunga Simba mara moja tu kwenye michezo mitano iliyopita kwa upande wa ligi, msimu wa mwaka 2012/2013 timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi na mzunguko wa pili Mei, 2013 Yanga ikashinda kwa goli 2-0 na kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya 24.
Msimu wa 2013/2014 watani wa jadi walitoka sare ya aina yake kwenye historia ya klabu hizo baada ya kutoka sare ya kufungana goli 3-3. Kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Yanga walimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa goli 3-0 lakini hadi firimbi ya mwisho ya mchezo huo matokeo yalikua ni 3-3.
Kwenye mchezo wa marudiano ambayo ilikua ni mechi ya mwisho ya ligi kuu msimu wa 2013/2014 uliopigwa Aprili 24, 2014 Yanga walilazimisha sare ya kufungana goli 1-1 goli la dakika za majeruhi kupitia kwa winga Simon Msuva likaiokoa Yanga kutoka kwenye kipigo cha ‘Mnyama’.
Octoba, 2014 Simba na Yanga zilitengeneza sare ye nne mfululizo kwenye mechi za ligi kwa misimu mitatu iliyopita baada ya kumaliza dakika 90 za mchezo huo kwa kutoka sare ya bila kufungana.
Kwa upande wa Simba Patrick Phiri ndiye kocha wa mwisho kuifundisha Simba ilipokutana na Yanga kwa mara ya mwisho katika mechi ya ligi. Kocha Mserbia Goran Kopunovic bado haja kiongoza kikosi cha Simba dhidi ya Yanga na kesho Jumapili itakuwa mara yake ya kwanza kuonja presha ya pambano la watani hao wa jadi pindi wanapokutana.
Kwa upande wao Yanga kocha wao Hans van der Pluijm bado hajakutana na Simba tangu arejee tena kwa mara ya pili kwenye klabu ya Yanga. Mbrazil Marcio Maximo, ndiye aliyekiongoza kikosi cha Yanga kilipokutana na Simba kwenye mchezo wa ligi na kutoka sare ya bila kufungana Octoba mwka 2014.
Pluijm yeye anafaida ya kuijua vizuri presha ya Simba na Yanga kwa sababu aliwahi kuiongoza Yanga kwenye michezo ya ligi dhidi ya Simba kabla hajaondoka kuelekea uarabuni kuifundisha timu ya Al Shaula FC ambayo baadaye aliachana nayo akiwa na msaidizi wake Charles Mkwasa.
Mchezo unaozikutanisha timu hizi kongwe za Tanzania hua una mambo mengi ndani na nje ya uwanja, tumeshuhudia mara kadhaa makocha wakitimuliwa baada ya kupoteza mechi dhidi ya Yanga au Simba. Lakini pia wachezajikutemwa’ au kushushiwa zigo la lawama pindi wafanyapo makosa yanayopelekea timu kufungwa, wakati mwingine wametuhumiwa kula ‘rushwa’ na kuiuza timu.
Lakini mashabiki nao wamekua wakipata wakati mgumu hasa pale timu zao zinapofungwa dhidi ya timu pinzani, mashabiki wa timu iliyofungwa hali huwa mbaya mtaani, nyumbani na hata kazini kwa kutaniwa na mashabiki wa timu iliyoshinda.
Lakini katika pambano la kesho Jumapili Yanga inapewa nafasi kubwa ya kushind mchezo huo kutokana na uimara wa kikosi walichokuwa nacho na ushiriki wa michuano ya Kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF.
Pamoja na udhaifu wa Simba lakini bado mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkali kwa pande zote mbili kutokana na upinzani wa timu hizo mbili kila zinapokutana na kibaya zaidi mara nyingi timu inayokuwa vizuri kama ilivyo Yanga kwa sasa ndiyo inayofungwa na ile iliyokuwa dhaifu.
Post a Comment