MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe ameithibitishia Mwanaspoti kuwa wamemtema rasmi kipa wao wa Uganda, Abel Dhaira na nafasi yake itachukuliwa na Ivo Mapunda.
Alisema baada ya kumsajili Yaw Berko wa Ghana, sasa wamemuongezea Mapunda ili kuimarisha lango.
Wakati hali ikiwa hivyo benchi la Ufundi la Simba limepigwa marufuku kuweka maji baridi katika mazoezi ya timu hiyo na hakuna mchezaji anayeruhusiwa kunywa maji hayo ili kulinda afya zao.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ndiye aliyeweka sheria hiyo na Mwanaspoti limeshuhudia meneja Nico Nyagawa akisisitiza kutowekwa maji hayo katika benchi lao.(P.T)
Katika mazoezi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Kinesi, jijini Dar es Salaam Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola aliomba maji kwa Nyagawa naye akaambiwa yapo ya moto ndipo Matola alipoulizia maji ya baridi.
"Kocha hataki maji ya baridi hapa, kama unataka kunywa ya moto sema nikupe," alisikika akisema Nyagawa akionekana kutekeleza agizo la Logarusic.
Baada ya kuona hali hiyo, Matola alikataa maji hayo na kuagiza aletewe maji ya baridi.
Ilibidi nahodha Nassor Masoud 'Chollo' ambaye hakufanya mazoezi kutokana na kuwa majeruhi, atoke nje ya uwanja huo kwenda kumtafutia Matola maji ya baridi ambayo aliyapata dakika chache baadaye.
Baadaye Logarusic aliliambia Mwanaspoti ni kweli amewapiga marufuku wachezaji wake kutumia maji hayo kwani ni hatari kwa afya zao wakiyatumia baada ya kuchemka mazoezini.
"Hali ya hewa ya hapa ni joto sana, haiwezekani mchezaji ametoka kuchemka halafu moja kwa moja unampa maji ya baridi hii ni hatari, nimewaambia sitaki kuyaona maji ya baridi hapa maana nataka kulinda wachezaji wangu," alisema Logarusic raia wa Croatia.
Timu kadhaa za Ligi Kuu Bara hata timu ya taifa hutumia maji ya baridi zinapokuwa katika mazoezi yao huweka maji hayo kwenye vyombo maalumu vya barafu.
Tangu kuwasili kwa kocha mpya wa Simba kumekuwa na utaratibu mpya katika kikosi hicho kuanzia mazoezi pamoja na maisha ya wachezaji kwa ujumla.Kocha huyo amesema anataka kuwa na kikosi cha wachezaji wasiozidi 25, lakini pia amekuwa akitaka wachezaji wanaojituma tu.www.skychami.com
Post a Comment