http://tropicalpoultryfarming.blogspot.com/

DAKIKA ZA LALA SALAMA DIRISHA DOGO LA USAJILI, OKWI ATUA YANGA RASMI!!




Emmanuel-Okwi580 (2)Unaona eeeh!: Wazee wa kazi wameshafanya yao, wamemnasa kijana Okwi, sasa kukipiga jangwani. Sakata lake, Yanga wadai wamefuatia hadi FIFA na wameshapata ITC

ZIKIWA zimesalia saa chache kabla ya kufungwa kwa pazia la usajili la dirisha dogo, mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans wametangaza kumsajili Emmanuel Anord Okwi  kwa mkataba wa miaka miwili.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb  amenukuriwa jioni ya leo akisema tayari wameshamsajili Okwi na sasa ni mali yao.
Kleb amesema taratibu zote zimekamilika na mshambuliaji huyo aliyewahi kutamba na Simba ataanza kuitumikia klabu hiyo mara mzunguko wa pili utakapoanza januari 25 mwakani.
“Tulimsajili Okwi takriban siku sita zilizopita, lakini Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imepatikana leo na ndiyo maana tumeamua kuweka mambo hadharani”. Alisema Bin Kleb.
Hata hivyo Bin Kleb amewahakikishia wana Yanga kuwa wamefika hadi FIFA,  na wameshawaona wanasheria kuhusu utata wa suala la Okwi na klabu yake ya Du Sahel, hivyo wapo sahihi kumsajili na ndio maana wamepata hadi ITC.
Okwi aliuzwa na Simba katika klabu ya Etoile Du sahel ya Tunisia januari mwaka huu kwa kitita cha dola 300, 000 za kimarekani, lakini hakudumu katika klabu hiyo kwa madai ya kutolipwa haki zake na kuamua kurejea kwao Uganda.
Okwi baada ya kurejea kwao Uganda alikaa miezi sita bila kucheza na ndipo shirikisho la  kandanda la Uganda (FUFA) likasimama kidete kumpigania aruhusiwe kureja nyumbani na kujiunga na Sport Club Villa ya Uganda `Majogoo wa Kampala`  ili kulinda kiwango chake.
Kwa usajili wa Okwi, Yanga imetimiza wachezaji watano wa kigeni kwa maana ya washambuliaji Didier Kavumbagu, Khamis Friday Kiiza, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima.
Sakata la Okwi lilifikishwa FIFA na mpaka sasa Etoile Du Sahel hawajailipa Simba Sc fedha za mauzo ya mchezaji huyo.
Mchezaji huyo mwenye akili kubwa ya mpira na kasi alikuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda katika michuano ya CECAFA Chellenge jijini Nairobi na kuonesha kiwango cha juu na sasa ametua Jangwani.
Yanga wamefanya usajili huo kwa lengo la kuimarisha kikosi chao kabla ya kuanza kampeni za ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani.
Mpaka sasa wametangaza kumsajili Juma Kaseja, Hassan Dilunga na leo hii Okwi imetia nanga katika rada zao.
      

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

CHARLES CHAMI. Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget