Rais wa zamani wa Yemen Jumamosi (21.02.2015) ametoroka kutoka
kifungo cha nyumbani cha wiki kadhaa mjini Sanaa nyumba yake ikiwa imezingirwa
na waasi wa Kishia
Washauri walio karibu naye wamesema kwamba Rais huyo wa zamani
Abd Raboo Mansour Hadi ameondoka Sanaa na tayari amewasili katika mji mkuu wa
iliokuwa Yemen ya kusini Aden ambapo wafuasi wake wamegoma kuyatambuwa mamlaka
ya baraza la rais lililowekwa na wanamgambo wa Kihouthi kuchukuwa nafasi yake.
Ameondoka mjini Sanaa akiwa kwenye msafara wa magari kadhaa kwa
kupitia mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo wa Taiz ambao kama vile Aden hauko
chini ya udhibiti wa waasi wa Kishia wa kundi la Wahouthi.
Afisa mwandamazi wa uslama mjini Aden ameliambia shirika la
habari la AFP kwamba Hadi mwenye umri wa miaka 69 anakaa kwenye kasri la rais
katika kitongoji cha kidiplomasia cha mji huo wa bandari wa Yemen kusini ambako
ndiko alikozaliwa.
Aliwababaisha walinzi
Washauri wake wanasema kwamba Hadi ambaye amekuwa kwenye kifungo
cha nyumbani kwa wiki kadhaa kufuatia mapinduzi ya waasi hao wa Kishia anapanga
kuondoka nchini kwenda nje kwa ajili ya matibabu.
Washauri hao wameongeza kusema kwamba waasi wamemuachia Hadi
kutokana na shinikizo kutoka Umoja wa Mataifa,Marekani,Urusi na vyama kisiasa
ndani ya nchi hiyo.
Hata hivyo mjumbe wa kamati kuu ya kundi la Wahouthi Ali
al-Quhum ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba Hadi alitoroka
kifungo hicho cha nyumbani kwa kuwakwepa walinzi kwa kuwababaisha.
Afisa huyo mwandamizi pia amekaririwa akisema hayo na tovuti ya
habari ya ndani ya nchi ya al-Akhbar na kuongeza kwamba hakuna tena maana iwapo
rais huyo wa zamani ameendelea kubakia hapo au kuondoka.
Wahouthi walivyodhibiti serikali
Wanamgambo wa kundi la Wahouthi ambao ngome yao kuu iko nyanda
za juu kaskazini wanakoishi Washia wengi waliuteka mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa
hapo mwezi wa Septemba bila ya upinzani.Mwezi uliopita waasi hao waliiteka
Ikulu na kuyazingira makaazi ya Hadi jambo lililopelekea rais huyo kujiuzulu.
Kwa mujibu wa mashahidi baada ya Hadi kuondoka kwenye makaazi
yake Wahouthi walifanya uporaji kwenye nyumba yake na kwamba watu watatu
walionekana wakitoka na bunduki za aina ya Kalashnikov kutoka kwenye nyumba
hiyo.
Jamal Benomar mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen amesema hapo
Ijumaa kwamba makundi yanayohasimiana nchini humo yamekubaliana kuunda baraza
jipya la kutunga sheria litakalojumuisha Wahouthi, wabunge wa zamani na wapya
kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito.
Lakini muungano wa vyama vya kisiasa nchini humo umeukataa
mpango huo kwa hoja kwamba haukidhi haja ya kuleta ufumbuzi kamili.
Ahmed Lakaz msemaji wa chama cha Mkusanyiko wa Vyama vya
Wafanyakazi ambacho kilikuwa kinashiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi
wa mzozo wa Yemen amesema kwamba vyama hivyo vimewaeleza Wahouthi kwamba
hawatashiriki katika mchakato huo iwapo Hadi hatoachiliwa.
Kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa
Yemen imetumbukia kwenye mzozo wa kisiasa tokea waasi wa kundi
la Wahouthi kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa na baadae kulazimisha kujiuzulu
kwa rais aliyechaguliwa anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi na kulivunja
bunge wakati wakimweka Hadi kwenye kifungo cha nyumbani.
Wakati huo huo waasi hao wa kundi la Wahouthi Jumamosi
walijaribu kuvamia kambi ya kikosi maalum ilioko nje ya mji mkuu na
kushambuliana kwa risasi na wanajeshi wa kikosi hicho ambao wengi wao ni tiifu
kwa Ali Abdallah Saleh mtangulizi wa Hadi.Kwa mujibu wa maafisa wa usalama
mapigano hayo yameuwa watu watatu.
Washauri wa Saleh wanasema kiongozi huyo wa zamani anaiona kambi
hiyo kuwa muhimu kwa uhai wake na kamwe hatoruhusu iangukie mikononi mwa
Wahouthi kama vile ilivyokuwa kwa vituo vyengine vya kijeshi ambavyo tayari
viko mikononi mwa Wahouthi. Washauri wake hao wamezungumza hayo kwa masharti ya
kutotajwa jina kutokana na kwamba Saleh hakuwaruhusu wazungumze na waandishi wa
habari.
Maandamano dhidi ya Wahouthi yaendelea
Maelfu ya watu pia wameandamana Jumamosi kumuunga mkono Hadi
katika mji wa kusini wajimbo la Ibb ambapo wamewataka Wahouthi kuondoka katika
eneo hilo na kuacha kuingilia kati masuala ya ndani ya jimbo hilo.Duru za
usalama zinasema Wahouthi waliwafyetulia risasi na kuuwa mwandamanaji mmoja na
kujeruhi wengine wawili.
Waasi hao wa kundi la Wahouthi walijipenyeza hadi kwenye maeneo
yanayokaliwa na Wasunni wengi kusini na magharibi mwa mji mkuu wa Sanaa ambapo
walikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa kikabila na wanamgambo
wa kundi la Al Qaeda.
Mji wa Taiz na baadhi ya sehemu nyengine za kaskazini
halikadhalika eneo zima la kusini mwa Yemen hayako chini ya udhibiti wa waasi
hao.
Mzozo
huo wa kisiasa nchini Yemen pia unauweka mashakani uwezo wa Marekani kuendeleza
operesheni zake za kupambana na ugaidi hususan kutokana na kuondolewa kwa Hadi
mshirika madhubuti wa Marekani.
Post a Comment