Mji wa Vatikani ni dola-mji lenye eneo la kilomita za mraba 0,44 tu. Hivyo ni nchi ndogo kuliko zote duniani. Pande zote inazungukwa na Italia.
Idadi ya wakazi ni 791; raia ni 565 tu (mnamo Oktoba 2008).
Ni nchi ya Papa ambaye ni askofu wa Roma na mkuu wa Kanisa Katolikiduniani kote.
Jina limetokana na kilima cha Vatikani (kwa Kilatini: Mons Vaticanus) ndani ya jiji la Roma, upande wa magharibi wa mto Tiber.
Pamoja na Basilika la Mt. Petro, jengo la kanisa kubwa kuliko yote duniani, Vatikani ina makanisa mengine saba, jumba la Vatikani, ofisi za utawala wa Kanisa Katoliki, mabustani, stesheni ya treni, nyumba za kuishi, hosteli kwa ajili ya mafukara na makumbusho yenye hazina kubwa za sanaa kiasi kwamba nchi nzima inahesabiwa na UNESCO kuwa Urithi wa dunia (tangu mwaka 1984).
Mji wa Vatikani ni mabaki ya Dola la Papa lililotawala sehemu kubwa ya Italia ya Kati kwa karne nyingi hadi 1870.
Tangu 1860 baadhi ya maeneo hayo yalitwaliwa na Ufalme mpya wa Italia uliolenga kuunganisha sehemu zote zapeninsula ya Italia.
Utawala wa Papa juu ya mji na mkoa wa Roma ulilindwa na Ufaransa hadi 1870.
Vita ya 1870 kati ya Ujerumani na Ufaransa ililazimisha Ufaransa kuondoa jeshi lake Roma, ambao hivyo ulitekwa na jeshi la Italia tarehe 20 Septemba 1870.
Wakati huo serikali ya Italia ilitaka kumuachia Papa Pius IX sehemu ya mji wa Roma kama eneo lake lakini Papa alikataa akitumaini Wakatoliki wa Italia na nchi nyingine duniani watalazimisha serikali ya Italia kumrudishia mji wote.
Kwa miaka 57 Mapapa walijifungia ndani ya jumba la Vatikani.
Mwaka 1929 serikali ya Benito Mussolini ilitafuta amani na Papa Pius XI aliyekuwa tayari kukubali mabadiliko.
Mkataba wa Laterani wa 11 Februari 1929 ukampa Papa mamlaka na madaraka ya nchi huru juu ya basilika la Mt. Petro pamoja na maeneo mengine.
Mkuu wa Dola ni Papa mwenyewe, kwa sasa Papa Fransisko (Jorge Mario Bergoglio). Nafasi yake ni kama mfalme wa kuchaguliwa asiyebanwa na katiba au masharti yoyote. Mambo ya utawala yako mkononi mwa gavana anayeteuliwa na Papa pia.
Vatikani ina uhusiano wa kibalozi na nchi 180 duniani kote kupitia Ukulu mtakatifu.
Vatikani ina jeshi dogo kabisa lakini lenye historia ndefu kabisa duniani. Ni kikosi cha Walinzi Waswisi ambacho kipo tangu mwaka 1506 na chenye wanajeshi 100 hivi. Wote ni Wakatoliki raia wa Uswisi kwa kuzaliwa.
Post a Comment