Wakimbizi wa Syria ambao ni sehemu ya jumla ya wenzao milioni 5 waliosambaa katika mataifa jirani kutokana na vita, ambavyo dunia imeshindwa kuvisimamisha. |
Shirika la Amnesty International limezikosoa serikali ulimwenguni kwa kushindwa kuwalinda mamilioni ya raia dhidi mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na makundi yenye silaha katika mwaka 2014.
Ripoti hiyo ya kila mwaka iliyochapishwa na shirika hilo la kutetea haki za binaadamu, inaelezea hatua ambazo zimechukuliwa na ulimwengu, kama vile kwenye migogoro nchini Nigeria na Syria kuwa ni za kutia aibu.
"Ripoti yetu kwa mwaka huu 2014/2015 inaelezea matukio ya kutisha ya ghasia na uvunjaji wa haki za binaadamu ambao watu kutoka Syria hadi Ukraine, Nigeria hadi Gaza wamekumbana nayo ndani ya kipindi hiki, lakini hatua za kukabiliana na matukio hiyo hadi sasa zimekuwa za ovyo na tuziita za kutia aibu," alisema Katibu Mkuu wa Amnesty International (AI), Salil Shetty, kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo jijini London siku ya Jumanne (Februari 24).
Mahsusi kabisa, Amnesty International inayalaumu mataifa tajiri duniani kwa kutumia nguvu na fedha nyingi kuwazuia watu kuingia kwenye mataifa hayo, kuliko kuwasaidia watu kuishi, ikiwemo kutumika vibaya kwa nguvu ya kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliundwa kwa lengo kuwalinda raia na kuhakikishia pana amani na usalama lakini limeshindwa vibaya. Kwa hivyo tunasema miongoni mwa mambo yanayochangia kushindwa huku ni kutumika vibaya kwa kura ya turufu kunakofanywa na wanachama watano wa kudumu wa Baraza hilo la Usalama mara kwa mara," alisema Katibu Mkuu huyo wa AI mbele ya waandishi wa habari.
Kwa hili, Shetty aliwatolea wito wanachama hao wa kudumu wa Baraza la Usalama - Marekani, Ufaransa, Urusi, China na Uingereza - kujizuia kutumia kura yao ya turufu, inapotokezea wametakiwa kupigia kura uvunjaji wa haki za binaadamu na matukio ya ghasia duniani.
Mauaji zaidi, ghasia zaidi, wakimbizi zaidi
Watu milioni 50 walilazimika kukimbia makaazi yao kwenye mwaka 2014, ambao AI imeuelezea kuwa mwaka uliokuwa na mauaji mengi zaidi yaliyofanywa na vyombo vya dola na makundi ya waasi katika nchi zaidi ya 35 duniani, zikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati na India.
Kwa upande mwengine, Amnesty International imesema inatiwa wasiwasi na namna serikali zinavyochukuwa hatua panapotokezea kitisho cha usalama, kwa namna ambavyo zinageukia uvunjaji wa haki za binaadamu na ghasia dhidi ya watu wasiohusika.Ripoti hiyo inatabiri kuwa kutakuwa na mauaji na ghasia zaidi katika mwaka huu, kutokana na kusambaa na kupata nguvu kwa makundi kama Boko Haram katika mataifa ya magharibi mwa Afrika na Dola la Kiislamu, IS, katika mataifa ya Kiarabu.
"....serikali zinageukia kwa mara nyengine kurejea makosa yaliyofanyika baada ya mashambulizi ya Septemba 11 ambapo hatua za jumla jamala zilichukuliwa kupitia sheria kandamizi za kupambana na ugaidi, kama tunavyoshuhudia Ufaransa, Denmark na nchi kadhaa za magharibi, na haraka haraka nchi zinazoendelea kama Kenya, Uturuki, Misri zinafuata kuweka sheria za kama hizo za kupambana na ugaidi," inasema ripoti hiyo.
Matokeo ya hali hiyo, inasema Amnesty International, kama vile ukosefu wa utulivu kwenye nchi kadhaa ni kiwango cha juu cha wakimbizi duniani kote.
Ripoti inasema wakimbizi milioni nne wamekimbia vita nchini Syria, huku asilimia 95 ya hao wakirundikana kwenye mataifa jirani, ambapo dunia haionekani kuwajali sana wakimbizi wa mashariki ya kati.
chanzo DW
Post a Comment