| |
Hii ni licha ya Jose Mourinho kusema awali kwamba alipendelea Mbrazil mwingine, Oscar, akicheza nambari 10 ambayo imekuwa ya Mhispania huyo.
Willian hakuanza kwa kishindo alipotua Stamford Bridge baada ya kutibua mpango wa kuhamia Tottenham Hotspur dakika za mwisho akitokea klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi Agosti.
Eden Hazard na Oscar wamekuwa wakipendelewa kuanza na meneja Mourinho kwenye muundo wake wa wachezaji watatu ambao hufanya mambo yao nyuma ya straika mmoja katika mpangilio wa klabu hiyo ya London wa 4-2-3-1.
Wiki chache zilizopita, hata hivyo, Willian mwenye miguu miepesi ameingiza nguvu mpya katika safu ya kati ya mashambulizi jambo ambalo limemfurahisha sana Mourinho na kusaidia kuinua Chelsea hadi nambari ya tatu kwenye jedwali, alama mbili nyuma ya viongozi Arsenal.
Meneja huyo amekuwa akiwapa Willian, Oscar na Hazard ruhusa ya kudhibiti mpira na pia kulinda, timu inapopoteza mpira.
Imechukua wachezaji hao watatu muda wa kubadilisha na kutimiza matakwa ya Mourinho lakini mkimbio wa ushindi wa mechi sita mfululizo ni ishara tosha kwamba mbinu hiyo inafanya kazi.
"Ni ukweli kwamba muda wangu mwingi nilipokuwa Shakhtar Donetsk nilicheza katika wingi na pia nikacheza kama Nambari 10 hapa na pale nikiwa huko,” Willian mwenye umri wa miaka 25 aliambia tovuti ya Chelsea (www.chelseafc.com) mapema mwezi huu.
"Mambo ni sawa hapa, wakati mwingine niko kulia, wakati mwingine kushoto, na pia kucheza Nambari 10.
“Kucheza Nambari 10 huhitaji uwezo wa kutafuta nafasi na kukimbia na mpira ifaavyo. Huna nafasi nyingi na kuna watu wengi waliokuzunguka unapocheza lakini ujuzi niliopata nikicheza kutoka kando husaidia sana,” alisema Willian mwenye nywele ndefu.
"Bado nazoea nafasi hiyo lakini sioni matatizo katika ninavyocheza sasa.”
KIPENZI CHA MASHABIKI
Mata ndiye kipenzi cha mashabiki Stamford Bridge, na alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mwaka Chelsea iliposhinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu wa 2011-12 na pia msimu uliopita waliposhinda Europa League chini ya mtangulizi wa Mourinho Rafa Benitez.
Hakuna anayetilia shaka uwezo wa mchezaji huyo Mhispania mfupi wa kimo na pia ujanja wake anapopata mpira lakini inaonekana kana kwamba katika macho ya Mourinho hana ile kasi na uwezo wa kukabili wapinzani na kuweka kizuizi kama anavyotaka kwenye wachezaji wake watatu wa kushambulia.
Magazeti ya Uingereza yalijaa uvumi Jumanne kwamba Mata huenda akajiunga na mabingwa wa ligi Manchester United, timu ambayo Chelsea ililaza 3-1 uwanjani Stamford Bridge Jumapili, kwa ada ya takriban pauni 37 milioni ($60.75 milioni).www.skychami.blogspot.com
Post a Comment